Philemon

1 aPaulo, mfungwa wa Al-Masihi Isa, pamoja na Timotheo ndugu yetu:

Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtendakazi mwenzetu,
2 bkwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:

3 cNeema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mwenyezi Mungu Baba yetu na Bwana Isa Al-Masihi.

Shukrani Na Maombi

4 dSiku zote ninamshukuru Mwenyezi Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu, 5 ekwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Isa na upendo wako kwa watakatifu wote. 6 fNaomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Al-Masihi. 7 gUpendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.

Maombi Ya Paulo Ya Kumtetea Onesimo

8 hHata hivyo, ingawa katika Al-Masihi ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda, 9 ilakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Al-Masihi Isa, 10 jnakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo,
Onesimo maana yake ni Wa manufaa.
aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.
11Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.

12Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa. 13 lNingependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili. 14 mLakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari. 15 nHuenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima. 16 oSi kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.

17 pHivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe. 18 qKama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi. 19 rNi mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa. Sitaji kwamba nakudai hata nafsi yako. 20 sNdugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Al-Masihi. 21 tNikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.

22 uJambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.

Salamu Za Mwisho Na Dua Ya Kuwatakia Heri

23 vEpafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Al-Masihi Isa, anakusalimu. 24 wVivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watendakazi wenzangu wanakusalimu.

25 xNeema ya Bwana Isa Al-Masihi iwe pamoja na roho zenu. Amen.
Copyright information for SwhKC